Mfumo wa stakabadhi ghalani wawanufaisha wakulima Chemba
7 September 2026, 17:09

Mfumo huo umepanua masoko na kuwawezesha wakulima kupata fedha taslimu kwa haraka na kwa wakati, huku ukisaidia wilaya kupata mapato yake kwa urahisi. Wakulima wametakiwa kuendelea kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuzingatia ubora wa mazao na taratibu zilizowekwa ili kunufaika zaidi na kuongeza kipato cha kaya zao.
Na Mathias Mgale.
Mfumo wa stakabadhi ghalani umetajwa kuendelea kuwanufaisha wakulima wilayani Chemba kwa kuwawezesha kuhifadhi mazao yao katika maghala salama na kuyauza wakati bei inapokuwa nzuri.
Baadhi ya wakulima wamesema mfumo huo umekuwa na umuhimu mkubwa, kwani pamoja na kuwasaidia kuhifadhi mazao kwa usalama, pia unawawezesha kupata fedha kupitia mazao yaliyohifadhiwa na kuuzwa kwa wakati na bei nzuri. Hata hivyo, wamesema baadhi ya wakulima bado hawana elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya mfumo huo.
Akizungumzia faida za mfumo huo, Afisa Kilimo wa Kata ya Mpendo wilayani Chemba, Maziku Ramadhani Shalua, amesema unawasaidia wakulima kuongeza thamani ya mazao yao, kupata masoko yenye ushindani na kupunguza changamoto ya walanguzi wanaonunua mazao kwa bei ya chini wakati wa msimu wa mavuno.