Dodoma FM

Jamii yatakiwa kuacha dhana potofu kuhusu chanjo ya polio

21 August 2026, 17:39

Wazazi na walezi kutumia fursa hiyo kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo bila hofu wala mashaka. Picha na Mtandao.

Kampeni hiyo inalenga kuhakikisha watoto wanapata kinga dhidi ya polio, huku jamii ikihimizwa kushiriki kikamilifu kwa kuwapeleka watoto kupata chanjo na kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa afya ili kufanikisha lengo la kuzuia ugonjwa huo.

Na Anwary Shabani.

Jamii imetakiwa kuondokana na dhana potofu kwamba chanjo zinazotolewa kwa watoto si salama kwa afya, badala yake imehimizwa kujitokeza kuwapatia watoto huduma hiyo ili kuwaongezea kinga na kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa polio.

Hayo yamesemwa na Magdalena Dinawi, Afisa kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu kwa Umma, wakati wa kampeni ya chanjo ya polio inayotolewa kwa njia ya matone, ambapo watoto walio chini ya umri wa miaka kumi ndio walengwa wakuu.

Amesema chanjo hiyo ni muhimu katika kuongeza kinga ya watoto dhidi ya polio na kuwataka wazazi na walezi kutumia fursa hiyo kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo bila hofu wala mashaka.

Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Chanjo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Victor Kweka, amesema kampeni hiyo inalenga kuwafikia zaidi ya watoto 200,000 wenye umri chini ya miaka kumi.

Amesema Halmashauri imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha watoto hao wanapatiwa chanjo, ikiwemo kupitia shule za awali na za msingi pamoja na maeneo mbalimbali wanakopatikana watoto hao.

Nao baadhi ya wazazi wameahidi kuwa mabalozi wazuri kwa kuwahamasisha wazazi wenzao kuhusu umuhimu wa chanjo, huku wakiahidi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma watakaofika katika mitaa mbalimbali kwa ajili ya zoezi hilo.

Sauti na Anwary Shabani.