VETA yaendelea kuimarisha ushirikiano na viwanda mbalimbali nchini
4 September 2026, 16:43

Hatua hiyo ya VETA kuimarisha ushirikiano na waajiri pamoja na kuongeza udahili wa wanafunzi inalenga kuhakikisha vijana na Watanzania wengine wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuwaongezea uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa.
Na Anwar Shabani.
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA inaendelea kuimarisha ushirikiano na viwanda pamoja na waajiri, kwa lengo la kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji ya soko la ajira na kuwawezesha Watanzania kupata fursa mbalimbali za ajira.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alipokuwa akizungumza katika Ofisi ya Idara ya Habari Maelezo iliyopo Mtumba jijini Dodoma, ambapo amesema hatua hiyo inalenga kuongeza tija ya mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Aidha, amesema VETA imeendelea kuongeza wigo wa udahili wa wanafunzi, ambapo hadi sasa jumla ya wananchi laki Moja kumi na sita elfu mia nne sitini na nane wameweza kudahiliwa kupata mafunzo, ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na mwaka wa masomo 2022/2023, ambapo wanafunzi elfu sitini na tisa mia tatu arobaini na saba walidahiliwa.
Kwa upande mwingine, CPA Kasore amesema Serikali imeendelea kugharamia sehemu kubwa ya mafunzo hayo, ambapo inatumia asilimia 80 ya gharama za mwanafunzi mmoja, huku asilimia 20 ikibaki kuwa mchango wa mwananchi anayepata mafunzo.