Dodoma FM

Ugumu wa maisha na ushawishi rika wapelekea wanafunzi kuacha shule

18 September 2026, 16:37

Pichani wanafunzi wanaozagaa barabarani wakati wa masomo kwa ushawishi wa marafiki na kupuuza masomo. Picha na mwananchi.

Vijana wametakiwa kuelewa kuwa mafanikio hayapatikani mijini pekee, bali wanaweza kutumia elimu na ujuzi wanaoupata kujiajiri na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao ya vijijini, pasipo kutegemea ajira pekee.

Na mathias mgale.

Umaskini wa familia, ushawishi wa marafiki pamoja na imani kuwa mijini kuna fursa nyingi zaidi za kiuchumi, vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazowapelekea baadhi ya vijana kukatisha masomo yao na kukimbilia mijini kutafuta fursa hizo.

Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa changamoto za kifedha katika familia ni miongoni mwa sababu zinazowafanya vijana kuacha shule na kuelekea mijini, wakiamini kuwa wanaweza kupata kazi na kipato cha kusaidia familia zao.

Kwa upande wake, Dorcas Shayo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mimi Ni Taa Girls Foundation, amesema ni muhimu wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kushirikiana kuwahamasisha vijana kuhusu umuhimu wa elimu na kuwasaidia kukabiliana na changamoto zinazoweza kuwafanya kuacha shule.

Ameongeza kuwa ushawishi kutoka kwa marafiki pamoja na misukumo kutoka kwenye mitandao ya kijamii, inachangia baadhi ya vijana kufanya uamuzi huo, kwani huambiwa kuwa mijini kuna fursa nyingi za ajira na biashara bila kuzingatia umuhimu wa kuendelea na masomo.

Simulizi ya Mathias Mgale.