Dodoma FM

Chaula asifu uboreshaji wa miundombinu kata ya Uhuru

8 June 2026, 17:35

Picha ni uboreshaji wa miradi ya miundombinu ya barabara katika Kata ya Uhuru, jijini Dodoma.Picha na Anwary Shaban.

Mradi huo wa ujenzi wa barabara unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9 na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi sita.

Na Anwary Shaban.

Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Mheshimiwa Alimwoni Chaula, amesifu utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara katika Kata ya Uhuru, jijini Dodoma, baada ya kufanya ziara maalumu ya kukagua maendeleo ya mradi huo leo.

Meya Chaula amesema kuwa ujenzi wa barabara ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku akisisitiza kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali, kila jiji linapaswa kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara ili kuboresha huduma kwa wananchi.

Sauti ya Alimwoni Chaula

Akizungumza na Dodoma FM mara baada ya ukaguzi huo, Meya Chaula pia ametoa wito kwa wananchi kuacha kufanya biashara ndani ya maeneo ya barabara na kuepuka kuweka bidhaa au vifaa vinavyoweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.

Aidha, amewataka wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya miundombinu hiyo na kuacha kupitisha magari makubwa yasiyoruhusiwa katika baadhi ya maeneo ili kulinda ubora wa barabara na usalama wa raia.

Kwa upande wake, mmoja wa wafanyabiashara wa jijini Dodoma, ndugu Peter Mushi maarufu kama Mzee Kidia, ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo, akisema kuwa hapo awali hali ya barabara ilikuwa changamoto kubwa kwa wafanyabiashara na wananchi, lakini sasa mazingira ya biashara na usafiri yanatarajiwa kuboreka zaidi.

Sauti ya Peter Mushi