Dodoma FM
Dodoma FM
11 May 2026, 17:19

Alieleza kuwa Serikali itakaa pamoja na sekta husika kupitia tathmini ya kina ili kufikia uamuzi utakaowezesha wananchi wa maeneo hayo kupata huduma ya umeme kwa urahisi zaidi, huku akisisitiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha maendeleo ya huduma za kijamii yanawafikia wananchi wote bila kuacha eneo lolote nyuma.
Na Mariam Kasawa.
Wananchi wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wamehakikishiwa kuwa Serikali inaendelea kuboresha huduma za msingi za maji na umeme ili kuhakikisha wananchi wa maeneo yote wanapata huduma hizo kwa urahisi na gharama nafuu.
Kauli hiyo imetolewa Mei 8, na Waziri Mkuu wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika stendi ya mabasi ya Kibaigwa, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, ambapo alisema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya maji kwa kununua mitambo ya kisasa ya uchimbaji visima kwa ajili ya kila mkoa tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo kulikuwa na mitambo mitatu pekee nchini.
Alisema hatua hiyo inalenga kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi hususan wa maeneo ya vijijini na pembezoni, sambamba na kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, akizungumzia suala la umeme, Waziri Mkuu alisema Serikali imepokea changamoto zinazowasilishwa na wananchi kuhusu baadhi ya vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na huduma ya umeme pamoja na gharama za uunganishaji katika maeneo yaliyoainishwa kama mijini ilhali hali halisi ya maisha bado inafanana na mazingira ya vijijini.