Dodoma FM

Zaidi ya Walimu 3,100 Wajisajili Shindano la Taifa la Stadi za Ufundishaji

3 June 2026, 16:59

Picha ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir akiongea na waandishi wa habari.Picha na Bennard Komba.

Aidha, shule zitakazotoa washindi wa kwanza katika maeneo ya Kusoma kwa Darasa la Awali, Kiingereza kwa Darasa la Kwanza na Ufaraguzi wa Zana kwa Darasa la Pili zitapatiwa vibao vya kielektroniki 100 vyenye thamani ya Shilingi milioni tano, hatua inayotarajiwa kuongeza matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza kuwa jumla ya walimu 3,153 wamejisajili kushiriki Shindano la Taifa la Nne la Stadi za Ufundishaji kwa Walimu wa Shule za Awali na Msingi pamoja na Shindano la Pili la Stadi za Ufundishaji kwa Walimu wa Shule za Sekondari Tanzania Bara.

Hatua hiyo inalenga kuendelea kuimarisha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi mbalimbali za elimu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari , jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa mashindano hayo itafanyika Juni 6, 2026 katika Ukumbi wa Maktaba Mpya wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Picha ni baadhi ya walio shiriki katika mkutano huo wa naibu waziri wa elimu na waandishi wa habari.Picha na Bennard Komba.

Mhe. Ameir amesema mashindano hayo yanatoa fursa kwa walimu kuonesha umahiri, ubunifu na matumizi ya mbinu bora za ufundishaji darasani, huku yakichangia utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA).

Amefafanua kuwa kati ya walimu 3,153 waliosajiliwa kupitia Mfumo wa National Teaching Skills Competition System (TSCS), walimu 1,263 walikamilisha masharti yote ya ushiriki kwa kuwasilisha video za ufundishaji pamoja na maandalio ya masomo kwa ajili ya tathmini.

Kwa mujibu wa Mhe. Wanu, mchakato wa tathmini umekamilika na orodha teule ya walimu watano bora imepatikana katika kila eneo la ushindani. Mgeni rasmi katika hafla hiyo anatarajiwa kuwa Profesa Riziki Shemdoe.

Amesema mshindi wa kwanza katika kila kundi atazawadiwa Shilingi milioni 2.5, cheti cha pongezi, cheti cha ushindi pamoja na kompyuta mpakato, huku shule anayofundisha ikipata projekta kwa ajili ya kuimarisha mazingira ya ufundishaji.