Adha ya maji Mwanawota Mpwapwa hali yazidi kuwa tete
8 July 2026, 17:33

Kufuatia hali mbaya ya wananchi wa Kijiji cha Mwanawota ya shida ya maji, wameiomba serikali kuharakisha utekelezaji wa mradi wa maji ili kuwanusuru na magonjwa ya mlipuko yanayowakabili na migogoro inayoendelea.
Na Stephen Noel.
Wananchi wa Kijiji cha Mwanawota Kata ya Wota Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, wanasema maisha yao yamekuwa magumu kutokana na adha ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwanawota Bi. Ashura Ngiliule amesema changamoto hiyo imedumu kwa miaka mingi na imeathiri afya na maendeleo ya kijiji hicho.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Mwanawota Mpwapwa, Dkt. Musa Dedan amethibitisha kuwa changamoto ya maji kijijini hapo imekuwa chanzo cha magonjwa ya mlipuko ya mara kwa mara.
Amesema wananchi wengi wa Wota wamekuwa wakipata magonjwa yanayotokana na maji machafu kama kichocho, kipindupindu na magonjwa ya kuharisha.