Msajili wa Hazina, Fitch Ratings watathmini mageuzi ya taasisi za umma
13 August 2026, 11:07

Kampuni ya Fitch Ratings ilitaka kufahamu namna ilivyobadilika kutoka kipindi ambacho baadhi ya mashirika ya umma nchini yalikuwa yakikabiliwa na changamoto za kifedha.
Na Mwandishi wa OTR
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) Agosti 11, 2026, ilifanya mazungumzo na kampuni ya Fitch Ratings Ltd ikiwa ni sehemu ya mapitio ya pili ya mwaka 2026 ya tathmini ya Fitch Ratings, katika mchakato unaohusisha taasisi mbalimbali za Serikali.
Mazungumzo hayo yanalenga kuwapa wachambuzi wa Fitch Ratings fursa ya kupata taarifa za kina kuhusu mwenendo wa uchumi wa Tanzania, utekelezaji wa sera za kibajeti na fedha, pamoja na mikakati ya Serikali katika usimamizi wa deni la Taifa.
Kwa upande wa OTR, mjadala ulijikita katika utendaji wa taasisi za umma, mageuzi yanayoendelea, vihatarishi vya kifedha, pamoja na mtiririko wa fedha kati ya Serikali na taasisi za Umma.
Mapema mwaka huu, Fitch Ratings iliendelea kuipa Tanzania daraja ‘B+’ kwa hadhi ya ulipaji wa madeni ya muda mrefu ya fedha za kigeni, ikitaja mwelekeo imara wa ukuaji wa uchumi na uwezo wa Serikali kukabiliana na changamoto za kifedha baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Fitch inakadiria kuwa uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 6 kwa mwaka 2026, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ya wastani wa asilimia 4.5 kwa nchi zenye daraja la ‘B’.
Katika muktadha huo, Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, aliyeongoza timu ya OTR, aliieleza timu ya Fitch kuhusu mageuzi yanayolenga kuboresha utendaji na ufanisi wa taasisi za umma, kuimarisha utawala bora na uwajibikaji, pamoja na kupunguza utegemezi wa taasisi hizo kwa Serikali.

Alisema ajenda ya mageuzi ya OTR katika kipindi cha miaka miwili iliyopita imeweka mkazo zaidi katika uongozi, usimamizi wa utendaji na uwajibikaji, ikiwemo kuboresha ubora wa Bodi na timu za menejimenti na kuimarisha tathmini za Bodi ili kubaini mapungufu ya ujuzi.
Bw. Mchechu alisema matokeo ya mageuzi hayo yanaendelea kuonekana katika mchango wa kifedha wa taasisi za umma kwa Serikali.
Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2026, taasisi zilizo chini ya Msajili wa Hazina zilichangia takribani Sh1.881 trilioni kwa Serikali kupitia gawio na michango mingine, ikilinganishwa na Sh1.028 trilioni katika mwaka wa fedha uliotangulia.
Mwelekeo huo unaongeza matumaini kwamba mageuzi yanayoendelea yataimarisha zaidi utendaji na uendelevu wa kifedha wa taasisi za umma, kuongeza mchango wao katika uchumi na mapato ya Serikali, pamoja na kuunga mkono juhudi pana za Tanzania za kudumisha uimara wa kifedha na kuboresha hadhi yake ya mikopo.
Taarifa zilizotolewa katika mazungumzo ya OTR na Fitch Ratings yatachangia katika tathmini pana ya kampuni hiyo kuhusu uwezo wa Tanzania wa kutimiza majukumu yake ya kifedha, ikiwa ni sehemu ya mapitio ya pili ya mwaka 2026 ya tathmini ya hadhi ya Tanzania ya ulipaji wa madeni ya Serikali.