Wataalamu Waonya Matumizi ya Miwani bila kupima
22 October 2026, 13:14

Dkt. Emmanuel amewashauri watu wenye matatizo ya macho kufika katika vituo vya afya kwa uchunguzi kabla ya kupewa miwani.
Na Daniel Njau.
Wananchi wametakiwa kuacha matumizi ya miwani ya urembo na miwani ya jua bila kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kuepuka madhara yanayo weza kuwakumba.
Baadhi ya wananchi wamesema kuwa mara nyingi wamekuwa wkitumia miwani ya jua na urembo bila kufahamu kuwa kufanya hivyo kunaathiri afya ya macho.
Dkt. Emmanuel Edmundi, mtaalamu wa macho na mtoa huduma katika duka la miwani la Eyelight jijini Dodoma, amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia miwani bila kufanyiwa uchunguzi au kufuata ushauri wa kitaalamu, huku wengine wakivaa miwani ya watu wengine bila kujua ni hatari kiafya.
Dkt. Emmanuel amewashauri watu wenye matatizo ya macho kufika katika vituo vya afya kwa uchunguzi kabla ya kupewa miwani pia amewataka wananchi kutambua kuwa maumivu ya kichwa na kizunguzungu yanaweza kupelekea tatizo la kuona .
Matumizi ya miwani ni muhimu katika kurekebisha matatizo mbalimbali ya kuona, lakini ni vema mtu akafahamu hali ya afya ya macho yake kabla ya kuanza kuitumia.
Mahitaji ya macho hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine, hivyo kutumia miwani isiyolingana na mahitaji hayo kunaweza kusababisha usumbufu kama maumivu ya kichwa, kizunguzungu au kuona kwashida.