Utunzaji wa mazingira ni kinga dhidi ya magonjwa
25 November 2026, 16:30

Usafi wa mazingira umetajwa kuwa hatua muhimu katika kuzuia kuenea kwa magonjwa na kulinda afya ya jamii, huku tabia ya baadhi ya watu kutofuata taratibu za utunzaji wa mazingira ikitajwa kuwa changamoto inayoweza kuongeza hatari ya maambukizi ya magonjwa mbalimbali.
Na Daniel Njau.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Taswira ya Habari wamesema uchafuzi wa mazingira unatokana na kutowajibika kwa baadhi ya watu katika maeneo wanayoishi, wakisisitiza kuwa juhudi za kudumisha usafi zinapaswa kuanzia ngazi ya mtu binafsi, familia na kuenea katika jamii ili kupunguza uwezekano wa kutokea kwa magonjwa.
Wananchi hao wameiomba Serikali pamoja na mamlaka zinazohusika kuendelea kutoa elimu na hamasa kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira, huku wakihimiza usimamizi madhubuti wa sheria na kanuni za usafi ili kuhakikisha wanaokiuka taratibu hizo wanachukuliwa hatua stahiki.
Kwa upande wake, mtaalamu wa afya, Bi. Magdalena Mgaya, amesema mazingira machafu pamoja na kutofuata kanuni za usafi wa mwili vinaweza kuongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa mbalimbali, ikiwemo magonjwa ya mfumo wa chakula. Amesisitiza umuhimu wa kunawa mikono kwa maji safi na sabuni, hasa kabla ya kula na baada ya kutoka chooni, akieleza kuwa elimu ya usafi ni muhimu zaidi kwa watoto katika kujikinga na maambukizi.