Dodoma FM

FDH Tanzania kulinda watu wenye ulemavu dhidi ya athari za El nino

13 October 2026, 11:01

Picha ni Mkurugenzi Mtendaji wa FDH Tanzania, Maiko Salali, akiwa na watendakazi kwenda kutoa msaada. Picha na Anwary Shabani.

FDH Tanzania imesisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema na ushirikiano wa jamii katika kuwalinda watu wenye ulemavu dhidi ya majanga, huku hatua za sasa zikilenga kupunguza hatari na kuhakikisha kundi hilo haliachwi nyuma katika juhudi za kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño.

Na Anwary Shabani.

Shirika la Foundation for Disabilities Hope (FDH) Tanzania limeanza kutoa msaada wa chakula na mahitaji muhimu kwa familia zenye watu wenye ulemavu walio katika mazingira magumu, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa FDH Tanzania, Maiko Salali, amesema watu wenye ulemavu ni miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa wakati wa majanga, hali iliyolifanya shirika hilo kuanza kutambua familia zenye uhitaji mkubwa na kuzipatia msaada wa mahitaji ya msingi.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha watu wenye ulemavu ambao familia zao hazina uwezo wa kutosha wa kununua na kuhifadhi chakula wanapata mahitaji muhimu na kuwa salama katika kipindi hiki cha tahadhari ya mvua hizo.

Picha ni vitu vilivyoandaliwa na Shirika la Foundation for Disabilities Hope (FDH) kwaajili ya msaada. Picha na Anwary Shabani.

Salali amewataka watu wenye ulemavu, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuchukua tahadhari mapema kwa kuhifadhi chakula katika hali salama, kuepuka maeneo hatarishi na kusafisha mazingira yanayoweza kuhatarisha maisha yao wakati wa mvua hizo.

Kwa upande wake, Meneja Mahusiano wa FDH Tanzania, Godfrey Mpunza, amesema tahadhari iliyotolewa na mamlaka inapaswa kuwa kichocheo kwa jamii kuanza maandalizi mapema badala ya kusubiri madhara yatokee.

Mpunza amesema watu wenye ulemavu wanaweza kukabiliwa na changamoto zaidi wakati wa majanga, hivyo ni muhimu kuhakikisha wanapata taarifa za tahadhari kwa wakati, msaada unaohitajika na mazingira salama yatakayowawezesha kujilinda dhidi ya athari za mvua hizo.

Simulizi na Anwary Shabani.