Dodoma FM

Serikali imetenga bilioni 5 kuwezesha vijana wabunifu wa Tehama

3 October 2026, 12:47

Picha ni Waziri wa mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe Angellah Kairuki, akizindua programu hiyo octoba 2 mwaka huu katika ofisi za wizara mji wa serikali Mtumba. Picha na wizara ya mawasiliamo.

Serikali imezindua programu ya kuwezesha mitaji kwa kampuni changa za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kwa kutenga shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuwawezesha vijana wabunifu, huku Tume ya Tehama ikitakiwa kukamilisha mwongozo wa ushiriki wa kampuni hizo katika zabuni za Serikali, hatua inayolenga kuongeza ushindani wa kampuni za Kitanzania ndani na nje ya nchi na kuchochea uchumi wa kidijitali.

Serikali imezindua programu ya kuwezesha mitaji kwa kampuni changa za Tehama ili kuwezesha na  kupata kampuni za kitanzania zenye uwezo wa kukua na kushindana ndani ya nchi na kimataifa.

Akizindua programu hiyo octoba 2 mwaka huu katika ofisi za wizara mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma Waziri wa mawasiliano na teknolojia ya Habari Mhe Angellah Kairuki amesema kuwa serikali imeweka mazingira wezeshi kuendeleza sekta ya Tehama ambapo imetenga shilingi bilioni 5 ili kuwezesha vijana wabunifu.

Mhe Kairuki ameiagiza tume ya Tehama kukamilisha mwongozo wa namna kampuni changa za Tehama zitakavyoweza kushiriki katika zabuni za serikali huku akiwataka wabunifu kutafakari umuhimu wa kuanzisha umoja wao rasmi kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu.

Sauti ya Waziri wa mawasiliano na teknolojia ya Habari Mhe Angellah Kairuki

Aidha mwenyekiti wa bodi ya tume ya Tehama Dkt Henry Mwanyika amesema tume imekuwa Daraja katika kuhakikisha dira ya maendeleo ya taifa 2050 inafikiwa ambapo imetaja mapinduzi ya kidijitali kama kichocheo kikuu cha Uchumi wa taifa.

Sauti ya Mwenyekiti wa bodi ya tume ya Tehama Dkt Henry Mwanyika.

Ikiwa haya yanafanyika wapo vijana wa kitanzania ambao wameonesha mfano kwa kubuni bunifu  zenye kutatua changamoto katika jamii,Yusuph Hamisi Mata ni miongoni mwa vijana hao.

Sauti ya Yusuph Hamisi.

Itakumbukwa kuwa Jun 27 mwaka 2025 katika hotuba ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani akihutubia bunge aliweka mkazo katika kuziwezesha na kulinda kampuni changa nchini.