Dodoma FM

Ushiriki wa wazazi watajwa kuimarisha malezi ya watoto

11 November 2026, 16:38

Picha ni wazazi wakishirikiana katika kumjenga mtoto katika maadili. Picha na Jamiiforum.

Ushiriki wa wazazi na walezi katika malezi ya watoto umetajwa kuwa nguzo muhimu katika kujenga familia imara na jamii yenye maadili mema, huku baadhi ya wananchi wakieleza kuwa kukosekana kwa muda wa kutosha wa kukaa na kuzungumza na watoto ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuathiri mwenendo na makuzi yao.

Na Daniel Njau.

Baadhi ya wananchi wamesema, baadhi ya wazazi wamekuwa wakiacha jukumu kubwa la malezi kwa wasaidizi wa kazi za ndani kutokana na shughuli mbalimbali za kutafuta maisha, hali inayoweza kupunguza ukaribu na mawasiliano kati ya wazazi na watoto.

Wamesisitiza kuwa ni muhimu wazazi kutenga muda wa kuwafuatilia watoto wao, kusikiliza changamoto zao na kuwapa mwongozo unaofaa katika hatua mbalimbali za ukuaji.

Kwa upande wake, Mtaalamu na Mshauri wa Malezi na Familia, Bi. Sadaka Gandi, amesema malezi ni mchakato mpana unaohusisha vitendo na juhudi mbalimbali zinazofanywa na mtu mzima katika kumwelekeza mtoto au kijana ambaye bado hajafikia hatua ya kufanya maamuzi yake binafsi.

Amesema wazazi na walezi wana nafasi kubwa katika kumjengea mtoto misingi ya nidhamu, uwajibikaji na uwezo wa kutofautisha mema na mabaya.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kushiriki katika vipindi na programu za elimu ya malezi ili kuongeza uelewa kuhusu namna bora ya kuwalea watoto kulingana na mahitaji ya ukuaji wao.

Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya wazazi, walezi, shule na jamii ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama, yenye upendo, uelewa na maadili mema yatakayowasaidia kuwa raia wema katika siku zijazo.

Simulizi na Daniel Njau.