Dodoma FM

Wananchi Dabalo waomba kuongezewa tenki la maji

25 September 2026, 16:50

Picha ni Tenki linalo saidia upatikanaji wa maji kwa jamii katika kutatua changamoto ya wana jamii kutembea umbali mrefu. Picha na DUWASA.

Kutokana na ongezeko la idadi ya watumiaji linalosababisha foleni na baadhi ya wananchi kulazimika kufuata huduma hiyo katika vijiji vya jirani. Wakazi hao wamesema kuongezwa kwa miundombinu hiyo kutasaidia kupunguza adha ya kutafuta maji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa urahisi na kwa wakati.

Na Victor Chigwada.

Wakazi wa Kata ya Dabalo, Wilaya ya Chamwino, wameomba kuongezewa tenki la maji ili kukidhi mahitaji ya wakazi wanaoongezeka katika eneo hilo.

Wamesema upungufu wa matenki na mabomba ya kuchotea maji umesababisha baadhi ya wananchi kutumia muda mwingi kupanga foleni ili kupata huduma hiyo.

Hali hiyo imewalazimu baadhi ya wananchi kufuata huduma ya maji katika vijiji vya jirani kutokana na huduma iliyopo katika eneo lao kutokidhi mahitaji ya wakazi.

Mwenyekiti wa Maendeleo wa Kata ya Dabalo, Omary Kiguna, amesema licha ya kuwepo kwa tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 150,000, idadi kubwa ya watumiaji imekuwa ikifanya tenki hilo kushindwa kukidhi mahitaji.

Kiguna ameongeza kuwa tayari hatua za kukabiliana na changamoto hiyo zimeanza kuchukuliwa, ambapo Shirika la World Vision linaandaa ujenzi wa tenki jingine pamoja na uchimbaji wa kisima kingine cha maji.

Simulizi na Victor Chigwada.