Vijana watakiwa kujiepusha na unywaji wa pombe ili kufikia malengo
2 October 2026, 16:41

Ongezeko la upatikanaji wa pombe mitaani na katika baadhi ya maeneo ya biashara pia limechangia baadhi ya vijana kujiingiza katika ulevi badala ya kutumia muda wao kufanya kazi na kujenga maisha bora ya baadae.
Na Victor Chigwada.
Wimbi la vijana wasiokuwa na shughuli za kuwaingizia kipato na kutumia muda mwingi kuzurura mitaani limetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa Idara ya Elimu wa Kanisa la Anglikana, Jimbo la Dodoma, Bi. Apaisalia Kiwoli, wakati akizungumza na vijana pamoja na wazazi wa Jimbo la Dodoma, ambapo amesema vijana wanaokosa shughuli za kuwaweka busy wanaweza kukosa mwelekeo na kuwa na mchango mdogo kwa familia na Taifa.
Kiwoli ameongeza kuwa hali hiyo inaweza kuwafanya baadhi ya vijana kujihusisha na mienendo na masuala ambayo jamii inayapinga, akiwataka vijana kuwa na shughuli za kuwaendeleza na wazazi kuongeza juhudi katika malezi na usimamizi wa watoto wao.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi wamesema mabadiliko ya teknolojia na mitandao ya kijamii yameathiri malezi ya vijana, hali inayowafanya wazazi kupata changamoto katika kuwafuatilia na kuwajenga kimaadili.