Dodoma FM

Wakulima watakiwa kuondoka eneo la malisho Kiteto

23 November 2026, 17:14

Picha ni wakulima wakiwa katika shughulli zao za kila siku mashambani. Picha na Dodoma Fm.

Wakulima wanaodaiwa kuvamia eneo la malisho la Alolle, lililopo katika Kijiji cha Amei, Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara, wametakiwa kuondoka mara moja ili kuepusha migogoro kati yao na wafugaji.

Na Hamisi Kitana.

Wakulima hao wanadaiwa kusababisha uharibifu wa mazingira kwa kufyeka misitu, kuchoma nyasi na kuandaa mashamba katika eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Remidius Mwema, kufuatia operesheni iliyofanywa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kwa lengo la kubaini wavamizi na hali ya uharibifu wa mazingira katika eneo hilo.

Akizungumzia suala hilo, Afisa Ardhi wa Wilaya ya Kiteto, Huruma Valency, amesema maeneo hayo ya malisho yametengwa kwa mujibu wa sheria na kutangazwa katika Gazeti la Serikali. Ameeleza kuwa anashirikiana na Diwani wa Kata ya Loolera, Sokoine Edward, kusimamia utekelezaji wa agizo hilo.

Kwa upande wao, baadhi ya wakulima, akiwemo Valentine Kimwaga, wamekiri kuvamia eneo hilo.

Hata hivyo, Katibu wa Chama cha Wakulima Wilaya ya Kiteto, Ezekieli Yohana, amesema baadhi ya wafugaji wamekuwa wakikodisha maeneo ya malisho kwa wakulima, hali inayochangia changamoto hiyo. Ameitaka mamlaka husika kufanyia kazi suala hilo ili kupata suluhisho la kudumu.

Ripoti ya Hamis Kitana.