Polisi Dodoma waendelea kuimarisha uhusiano na jamii kwa kutoa elimu ya usalama
26 August 2026, 17:03

Maadhimisho ya miaka 20 ya Polisi Jamii nchini yanaendelea chini ya kaulimbiu inayohimiza ushirikiano kati ya jamii na Jeshi la Polisi katika kudumisha amani, usalama na umoja wa kitaifa. Kupitia maadhimisho hayo, elimu kwa wananchi inaendelea kusisitizwa kuwa ni nyenzo muhimu katika kuzuia uhalifu na kujenga jamii salama.
Na Anwary Shabani.
Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Polisi Jamii mkoani Dodoma limeendelea kuimarisha uhusiano na jamii kwa kutoa elimu ya usalama, madhara ya ukatili wa kijinsia na namna ya kujikinga na vitendo vya uhalifu kwa wanafunzi na walimu wa Shule ya Msingi Mazengo.
Elimu hiyo imetolewa na Kaimu Afisa Polisi Jamii Mkoa wa Dodoma, ASP Regina Mtana, wakati wa ziara ya Polisi Jamii shuleni hapo, iliyofanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya Polisi Jamii nchini. Katika ziara hiyo, Polisi Jamii pia walishiriki katika zoezi la usafi shuleni.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kikuyu Kaskazini, Heri Hussen, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kuifikia Shule ya Msingi Mazengo katika kuadhimisha miaka 20 ya Polisi Jamii, akieleza kuwa uwepo wa Polisi Jamii umekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha usalama na kutoa elimu kwa wananchi.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mazengo, Rehema Nkungu, amesema wanafunzi na walimu wamepata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu usalama, akibainisha kuwa elimu hiyo imekuwa ikitolewa kwa mwendelezo na imewasaidia wanafunzi kujikinga na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Sanjari na hayo, baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wamesema elimu wanayopewa na Polisi Jamii imekuwa na manufaa katika kuwasaidia kutambua na kuepuka vitendo vya ukatili wa kijinsia, huku wakieleza kuwa uwepo wa Polisi Jamii shuleni umekuwa msaada mkubwa kwao.