Unene kupita kiasi waongeza hatari ya kupata magonjwa
24 September 2026, 17:06

Wataalamu wa afya wanaendelea kusisitiza umuhimu wa kudumisha mtindo bora wa maisha kwa kuzingatia ulaji unaofaa, kufanya shughuli za mwili mara kwa mara na kupata ushauri wa kitaalamu inapohitajika.
Na Husna Munis.
Unene kupita kiasi umeelezwa kuwa miongoni mwa changamoto za kiafya zinazoweza kuongeza hatari ya kupata magonjwa mbalimbali, huku wataalamu wakisisitiza umuhimu wa lishe bora na kufanya mazoezi ya mwili.
Dkt. Onesmo Faustine, mtaalamu wa afya kutoka Hospitali ya BOCHU jijini Dar es Salaam, amesema unene kupita kiasi unaweza kuongeza hatari ya kupata changamoto mbalimbali za kiafya, hivyo jamii inapaswa kuchukua tahadhari na kuzingatia afya zao.
Akizungumza na KM24 FM, Dkt. Faustine amewataka wananchi kuwa makini katika uchaguzi wa vyakula, kufanya mazoezi mara kwa mara na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya, akibainisha kuwa unene kupita kiasi unaweza kuhusishwa na hatari ya kupata magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga wameeleza changamoto zinazowakabili katika kuzingatia ulaji bora na kufanya mazoezi kama sehemu ya maisha yao ya kila siku.