Dodoma FM

TOSCI yabaini uwepo wa mbegu zilizokwisha muda wa matumizi Dodoma

24 November 2026, 17:42

Picha niwakati wa ukaguzi katika maduka ya Pembejeo Jijini Dodoma.Picha na TOSCI.

Kutokana na hali hiyo, ni muhimu kwa wauzaji wa pembejeo kuzingatia taratibu na viwango vilivyowekwa katika biashara ya mbegu, huku wakulima wakihimizwa kuhakiki muda wa matumizi na ubora wa mbegu kabla ya kufanya manunuzi ili kujikinga na hasara zinazoweza kujitokeza na kuhakikisha wanapata mavuno yenye tija.

Na Anwary Shaban.

Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imebaini uwepo wa mbegu za mazao zilizokwisha muda wa matumizi pamoja na nyingine zisizokidhi viwango vya ubora vilivyoidhinishwa, kufuatia ukaguzi wa kushtukiza uliofanyika katika maduka na maghala ya kuhifadhia mbegu mkoani Dodoma.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mdhibiti Ubora wa Mbegu kutoka Makao Makuu ya TOSCI, Kitta Josephat, amesema wamebaini pia baadhi ya wauzaji wa mbegu kutokuwa wamepatiwa mafunzo ya kikanuni yanayotolewa na taasisi hiyo, hali inayoweza kuwanyima wakulima ushauri sahihi kuhusu uchaguzi na matumizi ya mbegu bora.

Akifafanua athari za matumizi ya mbegu zilizokwisha muda wa matumizi, Mdhibiti Ubora wa Mbegu wa TOSCI Evatha Paul, amesema mbegu hizo zinaweza kushindwa kuota au kustawi vizuri na kusababisha wakulima kupata mavuno hafifu, jambo linaloweza kuathiri uzalishaji wa chakula na usalama wa chakula nchini.

Kwa upande wake, Advera Charles, ambaye ni muuzaji wa duka la pembejeo mkoani Dodoma, ameomba radhi kwa kuuza mbegu zilizokwisha muda wa matumizi, akieleza kuwa walikuwa wakiamini mbegu hizo bado zina uwezo wa kuota na kustawi.

Ripoti ya Anwary Shaban.