Wananchi walalamikia uhaba wa maji safi Igandu
15 October 2026, 16:46

Wananchi wa Kitongoji cha Ndugai, Kijiji cha Igandu, wameendelea kukabiliwa na adha ya ukosefu wa maji safi na salama, hali inayowalazimu kutumia maji ya visimani ambayo pia hunywewa na mifugo, huku akina mama wakitumia muda mwingi kutafuta maji kwa ajili ya mahitaji ya nyumbani.
Na Victor Chigwada.
Wakazi wa Kitongoji cha Ndugai, Kijiji cha Igandu, wameiomba Serikali kuharakisha utatuzi wa changamoto ya maji safi na salama, ambayo imeendelea kuwaathiri katika shughuli zao za kila siku, hususan akina mama wanaotumia muda mwingi kutafuta maji.
Wakazi hao wamesema kutokana na kukosekana kwa maji ya uhakika, wanalazimika kutegemea maji ya visimani na vyanzo vingine vinavyotumiwa pia na mifugo, hali inayozua wasiwasi kuhusu usalama wa maji wanayotumia kwa matumizi ya nyumbani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Igandu, Joyce Chiloweka, amesema changamoto hiyo imeendelea kuwa kero kwa wananchi licha ya juhudi zinazoendelea kufanywa na Shirika la Water Mission kuweka miundombinu ya maji safi na salama katika eneo hilo.
Amesema awali Serikali ilichimba kisima kwa ajili ya kuwapatia wananchi maji, lakini maji yaliyopatikana yalikuwa na chumvi na hivyo kushindwa kutumika kwa ajili ya kunywa.