Serikali yawataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za el-nino
2 September 2026, 16:24

Itakumbukwa kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa utabiri Agosti 18, 2026 kuhusu uwepo wa hali ya El-Niño yenye nguvu inayoweza kusababisha mvua kubwa na madhara mengine, hivyo maandalizi yanahitajika ili kupunguza athari na kutumia fursa zinazotokana na mvua hizo.
Na Yussuph Hassan.
Serikali imeelekeza umma kamati za usimamizi wa maafa na sekta mbalimbali katika ngazi zote kushirikiana na kuhakikisha wananchi wanapewa elimu juu ya kuchukua tahadhari dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa za El-Niño.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kufatia taarifa iliyotolewa na mamlaka ya utabiri wa hali hewa juu ya uwepo wa mvua za El nino.
Mhe kabudi amesema wananchi wanapaswa kuepuka kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo hatarishi, kuweka akiba ya chakula, kutumia mbinu bora za kilimo pamoja na kuchagua mazao na mbegu zinazofaa kwa msimu wa Vuli.
Aidha kwa wa upande wa fedha, Profesa Kabudi amesema makadirio ya Shilingi Bilioni 730 yaliyoainishwa katika Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Niño si fedha zilizotengwa moja kwa moja kwa matumizi ya El-Niño, bali ni makadirio ya rasilimali zinazohitajika kutekeleza shughuli mbalimbali kabla, wakati na baada ya madhara hayo.
Serikali pia imewataka Mikoa, Halmashauri, taasisi na wadau wote kutambua maeneo hatarishi, kufanya tathmini za vihatarishi, kuimarisha miundombinu muhimu, kuandaa maeneo salama ya makazi ya dharura na kuhakikisha vifaa vya uokoaji pamoja na mifumo ya mawasiliano vinakuwa katika hali ya utayari.