Tanzania na Ujerumani zatekeleza mradi wa maji wa Sh bilioni 60.7
22 June 2026, 16:41

Aidha Dkt Natu Amesema kuwa mradi huo utakuwa na mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa maeneo yatakayofikiwa.
Na Anwary Shaban.
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani imeingia makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa maji wenye thamani ya Sh bilioni 60.7, unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya Tunduma, Vwawa na Mlowo.
Mkataba huo umesainiwa kupitia ushirikiano wa Serikali ya Ujerumani na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), ambapo fedha hizo zitaelekezwa katika kuboresha miundombinu ya maji, kuongeza uzalishaji pamoja na kuimarisha mifumo ya usambazaji wa maji kwa wananchi katika maeneo hayo.
Ameyazungumza hayo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri wakati wa hafla ya utiaji saini, amesema kuwa mradi huo ni hatua muhimu katika jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na endelevu ya maji.
Bi Mwajuma Amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba, amesema kuwa msaada huo kutoka Serikali ya Ujerumani unaonesha kuendelea kuimarika kwa mahusiano ya maendeleo kati ya nchi hizo mbili.