Dodoma FM

Watanzania wametakiwa kuwa na utamaduni wa kuipa kipaumbele lugha ya kiswahili

1 July 2021, 2:22 pm

Na; Yussuph Hans.

Moja ya lugha iliyoenea katika Mataifa ya Afrika ni Kiswahili kutokana jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kukuza Lugha hiyo na haina budi kila Mtanzania kujivunia Lugha ya Kiswahili.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania BAKITA Bi Consolata Mushi wakati akizungumza na Taswira ya habari ambapo amesema kuwa lazima kuwe na utamaduni wa tanzania kuipenda lugha ya kiswahili kwa kuzungumza pasi na kuipa kipaumbele lugha nyingine.

Ameongeza kuwa baadhi ya watanzania wanakaoishi na kusoma sehemu mbalimbali Afrika huona aibu kuzungumza lugha ya kiswahili jambo ambalo halitoi matokeo chanya katika kukuza lugha hiyo.

Taswira ya habari imezungumza na Mwalimu wa Lugha ya Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Dkt. Stella Faustin , pamoja na baadhi ya Wanafunzi kufahamu fursa gani wanaziona baada ya kuhitimu Masomo yao ambapo wamesema kuwa licha ya lugha hiyo kuwa fursa kubwa ya kuunganisha jamii ya Mataifa, pia kumekuwa na uhitaji wa Wataalamu wa kufundisha lugha hiyo.

Lugha ya kiswahili imekuwa na umuhimu mkubwa duniani kwa ujumla, na hasa Afrika, kwa sababu ya kuenea kwake nchi mbali mbali, na kuunganisha watu wa makabila na nchi nyingine wakaweza kufahamiana kwa lugha moja.