Dodoma FM

Wizara ya Maji yasaini mkataba na SU-YAPI Engineering Consulting Inc

24 October 2023, 2:16 pm

Picha ni Katibu Mkuu wizara ya maji Prof Jamal Katundu akisaini mkataba huo.Picha na Seleman Kodima.

Mkataba umesainiwa 23 Oktoba,  ikiwa ni awamu ya kwanza, mradi ambao utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 312 kwa ujenzi wa Bwawa lenye ujazo wa lita za maji milioni  440.

Na Seleman Kodima

Wizara ya Maji imesaini mkataba wa mwaka mmoja na  kampuni ya SU-YAPI Engineering Consulting Inc. kwa ajili ya kufanya kazi ya usanifu wa ujenzi wa bwawa la Farkwa litakalojengwa katika wilaya ya Chemba, ambalo litanufanisha wakazi wa wilaya za Chemba, Chamwino, Bahi na Jiji la Dodoma.

Waziri wa Maji  Mhe. Jumaa  Aweso (Mb) ameshuhudia hafla hiyo na amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 312 ili kuondosha tatizo la maji katika  Wilaya nne za Mkoa wa Dodoma ili wakazi wake wapate majisafi, salama na yenye kutosheleza.

Mhe. Aweso amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Chemba kuwa, Wizara ya Maji itatekeleza mradi huo kwa kuwashirikisha wananchi ili wawe sehemu ya mradi na ujenzi ukamilike kwa wakati kama ilivyopangwa na Serikali.

Sauti ya Mhe. Jumaa  Aweso.
Picha ni katibu Mkuu wizara ya maji akibadilishana mkataba na mhandisi wa kampuni hiyo. Picha na Seleman Kodima.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira,  Mhe. Jackson Kiswaga,  Mbunge wa Jimbo la Kalenga, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia kwa kujitoa na kupeleka fedha  kiasi cha shilingi Bilioni 312 kwa ajili ya ujenzi wa  Awamu ya kwanza ya Bwawa la Farkwa.

Sauti ya Mhe. Jackson Kiswaga, 

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule akiongea katika Hafla hiyo amewaomba wananchi wa Wilaya ya Chemba kuwa na imani na serikali yao kwa kuwa tatizo la upatikanaji wa maji linaisha, kwani Serikali imedhamiria kumaliza kabisa changamoto ya uhaba wa maji kwa wakazi wa Wilaya ya Chemba.

Sauti ya Mh.Rosemary Senyamule .