Wadau waungana kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto
25 November 2026, 16:16

Kampeni hiyo inatekelezwa chini ya kaulimbiu isemayo, “Tuungane kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, jenga taifa imara lenye haki na usawa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050,” huku wadau wakihimizwa kuhakikisha mapambano hayo yanaendelea hata baada ya siku 16 li kulinda haki, utu na usalama wa wanawake na watoto katika jamii.
Na Anwary Shabani.
Wadau mbalimbali nchini wametakiwa kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya ukatili wa wanawake na watoto kwa kubaini changamoto za kijamii zinazochochea vitendo hivyo na kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana nazo, ikiwa ni sehemu ya kulinda haki na usalama wa makundi hayo kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainabu Athuman, wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto jijini Dodoma, ambapo amezitaka wizara, taasisi za serikali za mitaa, mashirika ya kimataifa na asasi za kiraia kushirikiana katika kutekeleza na kufuatilia afua za kupinga ukatili.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Eliakim Mwaswi, amesema matarajio ya kampeni hiyo ni kuona jamii inajengeka katika misingi ya haki, usawa na kutokomeza vitendo vya ukatili, hatua itakayochangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Khatibu Kazungu, amesema kampeni ya siku 16 ni fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano wa wadau katika kulinda haki za watoto, wanawake na kujenga jamii yenye haki na usawa.
Naye, baadhi ya wadau walioshiriki uzinduzi huo, wakiwemo wawakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), wameeleza dhamira yao ya kuendelea kuunga mkono juhudi za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupitia ushirikiano na utekelezaji wa mikakati mbalimbali inayolenga kujenga jamii salama.