Jamii yatakiwa kutambua haki za mtoto wa nje ya ndoa kisheria
28 September 2026, 17:00

Hali ya wazazi kutengana na mtoto kukosa mahitaji yake ya msingi inaweza kumfanya mtoto kukosa mahitaji muhimu kama elimu, matunzo na mahitaji mengine ya msingi, hivyo kusisitiza umuhimu wa wazazi wote kutekeleza wajibu wao kwa ajili ya ustawi wa mtoto.
Na Daniel Njau.
Watoto waliozaliwa nje ya ndoa wana haki sawa za msingi kama watoto wengine, ikiwemo kupata matunzo, malezi, elimu na haki ya kumiliki mali, kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, huku wazazi wote wawili wakitakiwa kushiriki katika kuhakikisha ustawi na maendeleo yao.
Akizungumza kuhusu haki za watoto hao, mwanasheria kutoka TAWLA Mkoa wa Dodoma, Bi. Grace Mbenje, amesema Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, Sheria Na. 21, inamtaka kila mtoto kupewa matunzo na malezi bila kujali mazingira aliyozaliwa. Amesema sheria hiyo haibagui watoto kwa misingi ya kuwa wamezaliwa ndani au nje ya ndoa, bali inatambua haki zao za msingi.
Kwa mujibu Kifungu cha Namba 41 cha Sheria ya Mtoto kinawataka wazazi wote wawili kushiriki katika malezi na ustawi wa mtoto, ikiwemo kuhakikisha anapata mahitaji muhimu kwa ajili ya ukuaji wake.
Ameongeza kuwa mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa pia ana haki ya kumiliki na kurithi mali kwa mujibu wa sheria kama ilivyo kwa watoto wengine.
Baadhi ya wananchi wamesema changamoto ya baadhi ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa kukosa haki zao hutokana na mzazi mmoja kutotimiza wajibu wake, hasa pale wazazi wanapotengana.