Wananchi Nguji walalamikia ubovu wa barabara
15 October 2026, 16:58

Ubovu wa barabara katika Kitongoji cha Nguji, Mtaa wa Mapinduzi A, umekuwa kikwazo kwa upatikanaji wa usafiri wa uhakika, huku wakazi wakilazimika kutumia pikipiki na bajaji zenye nauli kubwa na kuiomba Serikali kuboresha miundombinu hiyo ili kurahisisha usafiri na kupunguza gharama za maisha.
Na Victor Chigwada.
Wakazi wa Kitongoji cha Nguji, Mtaa wa Mapinduzi A, wameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya barabara katika eneo hilo, wakisema hali ya barabara ilivyo sasa inawaongezea gharama za usafiri na kuwanyima huduma ya uhakika ya usafiri wa umma.
Wamesema ubovu wa barabara hiyo umekuwa kikwazo kwa wamiliki wa daladala kutoa huduma katika mtaa huo, hali inayowalazimu wananchi kutegemea pikipiki na bajaji ambazo nauli zake ni kubwa ikilinganishwa na usafiri wa daladala.
Wananchi hao wameeleza kuwa kuboreshwa kwa barabara hiyo kungewezesha magari ya abiria kuingia katika eneo hilo na hivyo kuongeza upatikanaji wa usafiri na kupunguza gharama wanazotumia kufika maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Golden Mathayo, amesema kuendelea kuweka kifusi katika barabara hiyo bila kuiboresha kwa kiwango cha kudumu kunaweza kuisababishia Serikali hasara, kwa kuwa kifusi hicho huharibika baada ya muda mfupi.
Mathayo amesema ni vyema barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami ili kudumu kwa muda mrefu na kurahisisha usafiri kwa wananchi, akieleza kuwa kipande kinachohitaji kuboreshwa kina urefu wa kilomita 16, kuanzia Makao Makuu ya Jeshi hadi kuungana na barabara ya Hospitali ya Benjamin Mkapa.