Askofu Mlawi atoa wito wa mazungumzo kwa vyama vya siasa
12 November 2026, 16:27

Kuimarika kwa amani na mshikamano wa Taifa kunatajwa kutegemea zaidi utayari wa vyama vya siasa kutatua tofauti zao kupitia mazungumzo, huku viongozi wa dini wakisisitiza umuhimu wa kuweka maslahi ya Taifa mbele.
Na Anwary Shabani.
Vyama vya siasa nchini vimetakiwa kuweka tofauti zao pembeni na kukaa meza moja kwa ajili ya mazungumzo yatakayosaidia kutafuta suluhu ya changamoto zilizopo, badala ya kuendeleza misuguano inayoweza kuathiri mshikamano wa Taifa.
Wito huo umetolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Spiritual Pentecostal Church of Tanzania (SPCT), Dkt. Musa Mlawi, ambapo amevitaja vyama vya Chadema, ACT Wazalendo na CCM kuwa miongoni mwa vyama vinavyopaswa kushiriki katika mchakato wa maridhiano kwa kuzingatia mazungumzo na kuheshimiana.
Katika hatua nyingine, Askofu Mlawi amesisitiza umuhimu wa kulinda amani na utulivu nchini, akieleza kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya wananchi na inatoa mazingira mazuri kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara na utalii.
Amewataka wananchi kujiepusha na vitendo vya vurugu pamoja na makundi yanayoweza kuchochea uvunjifu wa amani, huku akihimiza mshikamano, umoja na kuheshimiana kama misingi ya kuendelea kujenga taifa.
Amesisitiza kuwa njia ya mazungumzo na maridhiano inapaswa kupewa nafasi katika kutatua tofauti zilizopo, ili kulinda amani, kuimarisha mshikamano na kuweka mazingira bora ya maendeleo ya taifa.