Wajawazito Wahimizwa Kuwahi Kliniki Kupunguza Hatari Wakati wa Ujauzito
19 August 2026, 17:12

Amesisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha mama na mtoto wanapata uangalizi unaostahili hadi wakati wa kujifungua.
Na Stephen Noel
Akina mama wajawazito wilayani Mpwapwa wametakiwa kuwahi kupata huduma za kliniki mara wanapobaini kuwa ni wajawazito, ili kusaidia kubaini mapema changamoto za kiafya na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa ujauzito.
Akizungumza na Taswira ya Dodoma FM, mmoja wa wauguzi katika Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, Bi. Aisha, amesema kuwahi kliniki humsaidia mama mjamzito kupata taarifa na huduma muhimu zinazohusiana na afya yake pamoja na afya ya mtoto aliye tumboni.
Amesema kupitia kliniki, mama mjamzito hufanyiwa uchunguzi mbalimbali unaosaidia wataalamu wa afya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na kubaini mapema viashiria vya matatizo yanayoweza kuhatarisha maisha ya mama au mtoto.
Bi. Aisha amewataka pia wajawazito kufuata maelekezo wanayopewa na wataalamu wa afya na kuhudhuria kliniki kwa wakati katika kipindi chote cha ujauzito.