Serikali kuweka mikakati ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi
12 June 2026, 17:31

Mradi wa Empowered II unatarajiwa kuongeza uelewa wa haki za wafanyakazi wa majumbani, kuimarisha ulinzi wao kazini pamoja na kukuza ushirikishwaji wao katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Na Anwary Shaban.
Serikali, wadau wa kazi na mashirika ya maendeleo wameendelea kuweka mikakati ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi wa majumbani nchini.
Hayo yamejiri jijini Dodoma katika ukumbi wa OSHA, wakati wa uzinduzi wa mradi wa Empowered II unaohusu wafanyakazi wa majumbani, ulioandaliwa na CVM kwa kushirikiana na CHODAWU na kufadhiliwa na Serikali ya Italia.
Akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi huo, mwakilishi kutoka Wizara ya Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Khatib Khalid Hamadi, amesema amefurahishwa na mafunzo na mijadala iliyotolewa, akibainisha kuwa kazi za majumbani ni ajira rasmi kama zilivyo ajira nyingine na zina mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii na uchumi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyakazi wa Majumbani Taifa, Zanin Athuman Juma, amesema uzinduzi huo ni fursa muhimu ya kutoa elimu kwa wafanyakazi wa majumbani kuhusu haki na wajibu wao. Amesema bado jamii imekuwa ikiwatizama wafanyakazi hao kwa mtazamo hasi, hali inayochangia changamoto mbalimbali ikiwemo kucheleweshwa au kunyimwa malipo pamoja na kutokuwa na mikataba ya kazi.
Naye mfanyakazi muhamiaji, Sada Ibrahim, amesema kuanzishwa kwa mradi huo kutasaidia kuleta mabadiliko chanya kwa wafanyakazi wa majumbani kwa kuwawezesha kupata mikataba ya kazi, kulindwa zaidi na kupata maslahi stahiki katika maeneo yao ya kazi.