Dodoma FM

15 wahitimu mafunzo ya Orbit welding machine Veta Dodoma

3 June 2026, 16:31

Picha ni wahitimu wa mafunzo ya teknolojia ya Orbital Welding Machine yaliyodumu kwa siku 21 . Picha na Anwary Shaban.

Kwa ujumla, mafunzo hayo yanatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha nguvu kazi yenye ujuzi wa kisasa nchini na kuandaa wataalamu watakaoweza kukidhi mahitaji ya sekta ya viwanda na miradi mikubwa ya maendeleo.

Na Anwary Shaban.

Wanafunzi 15 wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA kutoka mikoa mbalimbali nchini wamehitimu rasmi mafunzo ya teknolojia ya Orbital Welding Machine yaliyodumu kwa siku 21, katika hafla iliyofanyika katika Chuo cha VETA Mkoa wa Dodoma.

Akizungumza wakati wa mahafali hayo, Kaimu Mkurugenzi wa VETA, Angelus Ngonyani, amesema mafunzo hayo yatawezesha Tanzania kuwa na wataalamu wa ndani wenye uwezo wa kufanya kazi za uchomeleaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa, hatua itakayosaidia kuongeza ajira kwa vijana na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Sauti ya Angelus Ngonyani.

Ngonyani ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeendelea kusisitiza ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kuendeleza mafunzo ya ufundi stadi, akibainisha kuwa VETA imekuwa ikitekeleza kwa vitendo maono hayo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Sauti ya Angelus Ngonyani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya SESDCORP, Killian Nango, amesema teknolojia ya Orbital Welding inalenga kurahisisha kazi za uchomeleaji kwa kutumia mifumo ya kisasa inayoweza kuendeshwa kwa njia ya remote control, hususan katika uchomeleaji wa mabomba na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini.

Sauti ya Killian Nango,

Naye Mkuu wa Chuo cha VETA Mkoa wa Dodoma, Deodatus Orotha, amesema mafunzo hayo yamefadhiliwa na wadau mbalimbali wakiwemo EACOP, PCK, VETA na SESDCORP, na yatawajengea wahitimu uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kimataifa kupitia teknolojia ya kisasa ya uchomeleaji.

Sauti ya Deodatus Orotha.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wenzake, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ametoa shukrani kwa waandaaji na wafadhili wa programu hiyo, huku akiwahimiza vijana wengine kutumia fursa za mafunzo ya ufundi stadi ili kujiongezea ujuzi na kuongeza tija katika kazi zao.