Dodoma FM
Dodoma FM
13 May 2026, 16:12

Aidha, Wakili Onyango amesema pande zote mbili zimesaini hati ya makubaliano kama uthibitisho wa kuhitimisha rasmi mgogoro huo.
Na Mariam Kasawa.
Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Awamu ya Pili) imefanikiwa kumaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 20 kati ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kibaigwa mkoani Dodoma na mwananchi Leonard Masagasi.
Mgogoro huo ulihusisha madai ya Masagasi ya kupokonywa eneo lake na mamlaka hiyo, ambalo baadaye lilitumika kwa ujenzi wa Shule ya Msingi Sabasaba, hali iliyosababisha mvutano wa muda mrefu kati ya pande hizo mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msimamizi wa Kampeni hiyo wilayani Kongwa ambaye pia ni Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, George Daniel, amesema suluhu hiyo ni mfano wa mafanikio ya matumizi ya mbinu mbadala za utatuzi wa migogoro.
Naye Mwenyekiti wa Mji Mdogo wa Kibaigwa, Angelico Fundikira, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hiyo inayowezesha wananchi kupata haki zao bila gharama.