Dodoma FM
Dodoma FM
5 May 2026, 16:15

Aidha, Mkoa umeanzisha namba maalum ya kuripoti matukio ya ukatili, pamoja na kuweka kamera 106 za ulinzi (CCTV) katika barabara kuu za Jiji la Dodoma ili kuongeza ufuatiliaji na usalama wa jamii.
Na Mariam Kasawa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma inaendelea kuchukua hatua za kimkakati na zenye matokeo katika kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kwa kuunganisha juhudi za uwezeshaji kiuchumi, ulinzi wa kijamii pamoja na mifumo madhubuti ya utoaji huduma kwa waathirika.
Akizungumza kuhusu hatua hizo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema kuwa Serikali ya Mkoa imejipanga kuhakikisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia hayabaki kwenye mipango pekee bali yanatafsiriwa katika matokeo halisi kwa jamii.
Katika kuimarisha mifumo ya ulinzi, madawati nane ya jinsia na watoto yameanzishwa katika vituo vya polisi vya wilaya zote, yakilenga kutoa huduma rafiki na za haraka kwa waathirika. Sambamba na hilo, vituo vitatu vya huduma ya “mkono kwa mkono” vimeanzishwa ili kurahisisha msaada wa kisheria, ushauri nasaha na ufuatiliaji wa kesi.
Katika eneo la ulinzi wa mtoto, watu 101 wamepatiwa mafunzo ya kuwa walezi wa watoto walio katika mazingira hatarishi, huku makao 18 ya watoto yakiendelea kutoa huduma za hifadhi na malezi kwa waathirika wa ukatili ndani ya mkoa.