Dodoma FM

Udanganyifu watokea maombi ya Ualimu

25 May 2021, 11:30 am

Na; Yussuph Hans

Serikali imesema itachambua kwa kina maombi ya ajira kwa kada ya ualimu ili haki itendeke kufuatia kuibuka changamoto ya udanganyifu kwa baadhi ya Waombaji.

Hayo yamebainishwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh.Ummy Mwalimu wakati akijibu swali la Mbunge wa Longido Mh.David Kilusu aliyehoji Serikali haioni umuhimu wa kuajiri watumishi wanaojitolea katika maeneo yao ili kuziba pengo la uhaba wa Walimu.

Waziri Ummy amesema watatoa kipaumbele kwa Watumishi wanaojitolea laikini watafanya uchambuzi kwa makini ili kukabiliana na udanganyifu ambao umeanza kufanywa na baadhi yao.

Ameongeza kuwa Serikali itaangalia pia watumishi ambao wamemaliza muda mrefu kujitolea na hawajapata ajira, ambapo Serikali itatoa fursa sawa kwa Watumishi hao kutokana na muda wao wa kuajiriwa kupungua.

Kwa upande mwingine Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora Mh.Deogratias Ndejembi amesema mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF  utaendelea kwa kaya zinazotambuliwa kuwepo katika Mradi huo, huku akitoa onyo kwa Viongozi watakaobainika kuingiza kaya hewa.

Mh.Ndejembi alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mh.Maida Hamad aliyehoji mpango wa TASAF kwa Vijiji vilivyobaki wakati huu mradi huo ukiwa ukielekea mwishoni.

Bunge limeendelea leo Jijini Dodoma ambapo wabunge wanaendelea kujadili bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa fedha 2021/22 ambayo ni kiasi cha Shilingi bilioni 294.1.