Dodoma FM

Waziri wa Afya awataka maafisa ustawi wa jamii kuwasaidia wagonjwa waliopo nyumbani

26 August 2021, 2:02 pm

Na;Yussuph Hans.

Wakazi Mkoani Dodoma wamepongeza agizo la Waziri Wa Afya, Dkt Dorothy Gwajima kuwataka Afisa Ustawi wa Jamii kuwatambua na kuwasaidia Wagonjwa waliopo Nyumbani pasi na kupatiwa Matibabu.

Akizungumza na Taswira ya habari Mmoja wa Wakazi hao Monica Stan ambaye aliwahi kupata changamoto ya Matibabu kutokana na kipato chake hali ambayo ilisababisha kumuwia vigumu kupata Matibabu na amesema hali hiyo itasaidia kupunguza wimbi la Wagonjwa nyumbani.

Aidha amesisitiza wataalamu katika kada ya Afya kuwakopesha wagonjwa wenye changamoto za kiuchumi ili wapate Matibabu kwa wakati bila ya kuwabagua.

Juma lililopita Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akiwa Mkoani Mwanza alipomtembelea Mtoto Shamsa Ramadhan Yusuph aliepata changamoto ya kumuuguza Bibi yake na kushindwa kwenda shule, Waziri Gwajima aliwataka Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii Nchini kuibua changamoto za Jamii na kuzitafutia ufumbuzi.