Wizara ya maendeleo ya jamii yapokea mashauri ya ndoa 49573, 2025/2026
2 June 2026, 16:58

Kati ya mashauri hayo, 9,995 yalisuluhishwa na kufungwa, 8,036 yalipelekwa Mahakamani na mashauri 31,542 yanaendelea kusuluhishwa.
Na Bennard Komba.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema wizara hiyo imepokea jumla ya mashauri elfu 49 na mia tano sabini na tatu ya ndoa katika kipindi cha Julai mwaka 2025 hadi Aprili mwaka 2026.
Dkt. Gwajima aliyasema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya mapitio ya utekelezaji wa mpango wa bajeti ya mwaka 2025/2026 pamoja na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2026/2027.
Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya waziri mkuu tawala za mikoa na serikali za mitaa ilipokea mashauri 49,573 ya ndoa.
Aidha, Waziri Gwajima amesema kati ya mashauri hayo, mashauri elfu 9 na mia 995 yalisuluhishwa na kufungwa, huku mashauri elfu 8 na 36 yakipelekwa mahakamani.
Ameongeza kuwa mashauri elfu 31 na mia 542 bado yanaendelea kusuluhishwa.