Wananchi watakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto
21 July 2026, 17:09

Aidha, amesisitiza kuwa si salama kwa mtu mmoja kujaribu kuzima moto peke yake kwa kuwa moto husambaa kwa kasi na unaweza kuhatarisha maisha.
Na Daniel Njau.
Wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto kwa kufuata kanuni za usalama na kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pindi moto unapotokea, ili kuokoa maisha na mali.
Akitoa elimu kuhusu majanga ya moto Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Aman Hassan amesema moto hutokana na mgongano au msuguano wa kikemikali ambapo joto, mwanga na hewa vinapokutana husababisha moto kuwaka.
Ameongeza kuwa shughuli mbalimbali za kijamii pia zinaweza kuwa chanzo cha milipuko ya moto, hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini na kufuata taratibu za usalama katika mazingira wanayoishi na kufanyia kazi.
Badala yake, amewataka wananchi kutoa taarifa haraka kwa kupiga simu namba 114 ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kupata msaada wa kitaalamu, pamoja na kuweka vifaa maalumu vya kutoa alama ya tahadhari ya moto katika majengo na maeneo ya kazi ili kurahisisha uokoaji pindi dharura inapotokea.