Kilimo cha nyanya chatajwa fursa ya ajira kwa vijana
31 August 2026, 17:29

Ili vijana waweze kufaidika kikamilifu na fursa hii, jamii inapaswa kuwapa ushirikiano na kuwatia moyo, huku serikali na wadau wengine wakiendelea kuboresha mazingira ya miundombinu ya kilimo na masoko.
Na Derick Mazemba.
Kilimo cha nyanya kimekuwa kikitajwa kama moja ya fursa muhimu zinazoweza kuwakomboa vijana kiuchumi na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.
Hata hivyo, mafanikio katika sekta hii yanahitaji uthubutu, maarifa sahihi, na matumizi bora ya mbinu za kisasa za kilimo ili kuepuka hasara.
Baadhi ya vijana wanao jihusisha na kilimo cha Nyanya katika eneo la Mpunguzi wanasema kilimo hiki kinalipa na kinaweza kubadilisha maisha, iwapo kijana atazingatia kalenda ya kilimo, kufanya utafiti wa soko kabla ya kulima, na kuwa mvumilivu anapokumbana na changamoto mbalimbali shambani.
Akizungumza kuhusu mbinu bora za kilimo cha nyanya, Afisa Kilimo wa kata ya Mpunguzi Bw. Fransis Chigwada amesema ni muhimu kwa vijana kuzingatia ushauri wa kitaalamu kuanzia hatua ya utayarishaji wa shamba, uchaguzi wa mbegu bora zinazostahimili magonjwa, hadi matumizi sahihi ya mbolea na viuatilifu.
Aidha, amewataka vijana kuacha kulima kwa mazoea na badala yake waone kilimo kama biashara. Amewashauri kuunda vikundi vya ushirika ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo ya pembejeo na kuongeza nguvu ya pamoja katika kutafuta masoko ya uhakika.