Unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni muhimu katika ukuaji na afya ya mtoto
5 August 2026, 12:49

Wiki ya Unyonyeshaji Duniani huadhimishwa kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 7 Agosti, ambapo Tanzania imekuwa ikiadhimisha wiki hiyo tangu mwaka 2002 kwa lengo la kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama katika afya, ukuaji na maendeleo ya mtoto.
Na Leokardia Andrew.
Wataalamu wa lishe wameendelea kusisitiza umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama, wakieleza kuwa mtoto mwenye umri wa chini ya mwaka mmoja anayenyonyeshwa ipasavyo na kupata lishe ya kutosha anapaswa kuongezeka uzito wa wastani wa angalau nusu kilo kwa mwezi.
Unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni muhimu katika ukuaji na afya ya mtoto, hasa katika miezi sita ya mwanzo ya maisha. Hata hivyo, baadhi ya wazazi wamekuwa hawazingatii utaratibu sahihi wa kuwanyonyesha watoto wao, hali inayoweza kuathiri ukuaji na afya ya mtoto.
Katika kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji, Afisa Lishe kutoka Hospitali ya Wilaya Kahama mkoani Shinyanga, Andrew Kasuka, katika mahojiano na KM24 FM amesema kuwa maziwa ya mama ndiyo lishe bora kwa mtoto katika miezi sita ya kwanza, kwani husaidia ukuaji wa mtoto na kuimarisha kinga ya mwili.
Kasuka amewataka wanawake kuwanyonyesha watoto wao mara kwa mara na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kuhakikisha watoto wanapata virutubisho muhimu vinavyohitajika kwa ukuaji bora.
Kwa mujibu wa Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator Survey (TDHS-MIS) 2022, asilimia 64.3 ya watoto wenye umri wa chini ya miezi sita nchini Tanzania hunyonyeshwa maziwa ya mama pekee, huku asilimia 70.2 ya watoto wakianza kunyonya ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa. Takwimu hizo zinaonesha hatua zinazopigwa katika kuhamasisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama nchini.
Wiki ya Unyonyeshaji Duniani huadhimishwa kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 7 Agosti, ambapo Tanzania imekuwa ikiadhimisha wiki hiyo tangu mwaka 2002 kwa lengo la kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama katika afya, ukuaji na maendeleo ya mtoto.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Mwanzo Imara wa Maisha ya Mtoto , Huanza na Maziwa ya Mama.”