Dodoma FM

Mikataba ya ajira yasisitizwa kulinda haki za wafanyakazi

24 September 2026, 16:34

Picha ni vitabu vya sheria, waajiri wakitakiwa kuzingatia umuhimu wa mikataba mahali pa kazi ili kulinda haki za mwajiriwa. Picha na mwananchi.

Ukosefu wa mikataba ya maandishi ya ajira umeendelea kuwa changamoto katika baadhi ya maeneo ya kazi, hali inayoweza kufanya wafanyakazi kupata ugumu kudai haki zao pindi migogoro inapotokea.

Na Daniel Njau.

Uwepo wa mikataba ya ajira bado ni changamoto katika baadhi ya maeneo ya kazi, huku baadhi ya waajiri na wafanyakazi wakikosa uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa mikataba hiyo katika kulinda haki na wajibu wa pande zote.

Baadhi ya wananchi wamesema elimu zaidi inahitajika kuhusu umuhimu wa mikataba ya ajira ili kuwafikia watu wengi katika jamii na kuwasaidia kutambua haki zao za msingi, hasa wanapokuwa katika mazingira ya kazi.

Kwa upande wake, Mwanasheria Enock Kiguha amesema Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini inasisitiza umuhimu wa kuwa na mikataba ya ajira kwa maandishi, ingawa makubaliano ya mdomo yanaweza pia kutambuliwa kama mkataba wa ajira.

Amesema hangamoto kubwa hujitokeza pale mzozo unapotokea na kuhitajika ushahidi wa makubaliano yaliyofikiwa, kwani kutokuwepo kwa mkataba wa maandishi kunaweza kufanya mchakato wa kuthibitisha makubaliano na kutatua mgogoro kuwa mgumu.

Simulizi na Daniel Njau