Maudhui ya mitandao ya kijamii yatajwa kuchochea mmomonyoko wa maadili
20 November 2026, 15:51

Wazazi, walezi na jamii wametakiwa kurejesha na kuimarisha misingi bora ya malezi kwa kushirikiana katika kuwafundisha watoto nidhamu, heshima na uwajibikaji, huku wakisimamia matumizi sahihi ya teknolojia ili kujenga kizazi chenye maadili mema na kinachoweza kukabiliana na mabadiliko ya dunia ya sasa.
Na Daniel Njau.
Matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii pamoja na udhaifu katika malezi ya watoto yametajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia mmomonyoko wa maadili katika jamii, huku wazazi na walezi wakihimizwa kuongeza usimamizi kwa watoto ili kuwajengea misingi bora ya nidhamu na uwajibikaji.
Baadhi ya wananchi wamesema mmomonyoko wa maadili unachangiwa kwa kiasi kikubwa na kukosekana kwa uangalizi wa karibu wa watoto majumbani, pamoja na baadhi ya wazazi kutotimiza ipasavyo wajibu wao wa kuwaongoza watoto katika kutambua mema na mabaya.
Kwa upande wake, mshauri wa malezi na familia, Dastan Haule, amesema baadhi ya wazazi wamekuwa sehemu ya changamoto hiyo kutokana na kutotekeleza ipasavyo wajibu wao wa malezi, huku maendeleo ya utandawazi yakileta mazingira mapya yanayohitaji uangalizi zaidi.
Hata hivyo, wananchi hao wameeleza kuwa kukabiliana na hali hiyo kunahitaji ushirikiano wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla, kwa kuhakikisha watoto wanapata elimu ya maadili tangu wakiwa wadogo, wanafuatiliwa katika matumizi ya mitandao ya kijamii na wanapatiwa mwongozo unaowawezesha kutofautisha maudhui yenye manufaa na yale yanayoweza kuathiri mwenendo wao.