Dodoma FM

Wazazi waomba mashine ya kudurufu mitihani shule ya sekondari Mtumba

6 October 2026, 16:46

Picha ni mashine ya kudurufu mitihani (kuchapisha nakala aza mitihani). Picha na masumi production.

Shule ya Sekondari Mtumba jijini Dodoma wameiomba Serikali na wadau wa elimu kusaidia upatikanaji wa mashine ya kudurufu mitihani, wakisema ukosefu wa kifaa hicho kwa muda mrefu umekuwa ukiwalazimu kuchangia gharama za mitihani ya ndani na hivyo kuongeza mzigo wa kifedha, hususan kwa wazazi wenye watoto zaidi ya mmoja.

Na Victor Chigwada.

Wazazi wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Mtumba, jijini Dodoma, wameiomba Serikali na wadau wa elimu kusaidia upatikanaji wa mashine ya kudurufu mitihani, wakisema kukosekana kwa kifaa hicho kwa muda mrefu kumekuwa changamoto na kuwaongezea mzigo wa kuchangia gharama za mitihani ya ndani ya shule.

Wamesema hali hiyo inawafanya kuchangia fedha kwa ajili ya kuandaa mitihani, jambo ambalo linakuwa changamoto zaidi kwa wazazi wenye watoto zaidi ya mmoja shuleni hapo.

Wameeleza kuwa, licha ya elimu kutolewa bila ada, ukosefu wa baadhi ya vitendea kazi unawalazimu wazazi kugharamia huduma ambazo shule inahitaji, hivyo kuiomba Serikali kutatua changamoto hiyo ili kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia.

Aidha, Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Godfrey Mseti, amesema hivi karibuni shule hiyo iliahidiwa kutatuliwa changamoto hiyo wakati wa Mahafali ya 19, kupitia Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Ndugu George Otione.

Mseti amesema ahadi hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Katibu Mkuu huyo katika mahafali hayo, Bi. Apaisalia Kiwoli, ambaye alisema suala hilo litafanyiwa kazi kwa uzito ili changamoto hiyo ibaki kuwa historia.

Simulizi na Victor Chigwada.