Elimu ya haki za watoto ni silaha dhidi ya ukatili
25 November 2026, 17:08

Elimu kuhusu ukatili wa kijinsia inayotolewa kwa watoto shuleni imetajwa kuwa nyenzo muhimu katika kuwajengea uwezo wa kutambua vitendo vya ukatili, kujilinda dhidi ya vitendo hivyo pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapokumbana navyo.
Na Mwanaidi Mpetu.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Dodoma FM wamesema elimu hiyo ni muhimu kwa watoto kwani huwasaidia kufahamu haki zao, kutambua aina mbalimbali za ukatili, ikiwemo unyanyasaji wa kingono, vitisho na ubaguzi, pamoja na kujua namna na maeneo sahihi ya kuripoti matukio hayo ili hatua stahiki zichukuliwe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Dodoma Mjini, ASP Loveness Mndeme, amesema elimu hiyo inapaswa kutolewa kwa kuzingatia umri na mazingira ya watoto ili waweze kuelewa ujumbe unaowasilishwa na kuutumia katika maisha yao ya kila siku. Amesema elimu hiyo huwasaidia watoto kutambua viashiria vya ukatili, kujilinda na kuwa na ujasiri wa kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo hivyo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya walimu, wazazi, walezi na vyombo vinavyohusika na ulinzi wa watoto katika kuhakikisha elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia inatolewa kwa endelevu, huku akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kujenga mazingira salama kwa watoto na kupunguza vitendo vya ukatili dhidi yao.