Chemba yaongeza maandalizi kukabiliana na athari za El Nino
29 October 2026, 17:15

Mvua kubwa zinazoweza kusababisha mafuriko, kuharibu miundombinu na kuathiri shughuli za kiuchumi zinahitaji maandalizi ya mapema ili kupunguza madhara kwa wananchi. Hali hiyo imeifanya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma kuimarisha mikakati ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza, ikiwemo kuziimarisha kamati za maafa, kuandaa maeneo ya kukabiliana na dharura na kutoa elimu kwa jamii kuhusu tahadhari za kuzingatia.
Na Kitana Hamisi.
Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Aziza Mangosongo, amezitaka kamati za maafa katika vijiji vya Mpendo, Kubi, Hamia na Magungu kuimarisha maandalizi na kutekeleza majukumu yao ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha.
Wito huo umetolewa wakati wa ziara yake katika Kata ya Mpendo, ambapo alikagua maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kukabiliana na dharura na kufanya kikao na viongozi wa serikali za vijiji pamoja na wajumbe wa kamati za maafa.
Katika kikao hicho, Mangosongo amewataka viongozi na wananchi kuzingatia tahadhari za maafa, kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na athari za mvua kubwa, pamoja na kutunza mazingira na miundombinu ya maendeleo.
Aidha, amewapongeza wananchi kwa kukusanya zaidi ya tani moja ya chakula na kuandaa miundombinu ya kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.
Maandalizi hayo pia yanahusisha juhudi za kutatua migogoro kati ya wakulima na wafugaji ili kuimarisha usalama na mshikamano wa jamii wakati wa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.
Hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Wilaya ya Chemba kuimarisha utayari wa wananchi na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa.