Dodoma FM

Elimu ya uzazi yatajwa kuwa kinga kwa mama na mtoto

17 November 2026, 15:31

Picha ni kina mama wajawazito wakiwa wanahudhuria kliniki kwaajili ya kupata elimu na maendeleo ya mtoto aliye tumboni. Picha na Habari leo.

Familia na jamii kwa ujumla zimetakiwa kuzingatia umuhimu wa kupata elimu ya afya ya uzazi na kupanga uzazi kwa kutumia njia salama zinazotambulika kitabibu, huku wanawake wakihimizwa kuhudhuria kliniki na kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya kupata ushauri na huduma stahiki kwa wakati.

Na Daniel Njau.

Elimu ya afya ya uzazi imetajwa kuwa muhimu katika kulinda afya ya mwanamke na mwenza wake, hususan katika kipindi cha kujiandaa kupata ujauzito, wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua, ili kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza katika hatua mbalimbali za uzazi.

Hata hivyo, baadhi ya wanawake bado wanakabiliwa na changamoto zinazowafanya kusita kufika katika vituo vya afya kupata huduma za afya ya uzazi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni hofu zinazohusiana na umri pamoja na namna wanavyopokelewa na baadhi ya wahudumu wa afya, hali inayoweza kuwakatisha tamaa na kuwafanya washindwe kupata ushauri sahihi wa kitaalamu.

Akizungumzia suala hilo, mtaalamu wa afya ya uzazi kwa wanawake, Bwana John France, amesema huduma za afya ya uzazi zina mchango mkubwa katika kumsaidia mama mjamzito kufuatilia maendeleo ya ujauzito na kuhakikisha usalama wake pamoja na mtoto aliye tumboni.

Ameongeza kuwa ukosefu wa elimu sahihi kuhusu uzazi wa mpango ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili baadhi ya wanawake.

Ripoti na Daniel Njau.