Wananchi waiomba serikali kuweka mpango wa kukabiliana na majanga
7 October 2026, 17:08

Wananchi wameiomba Serikali kuandaa maeneo ya muda ambayo yanaweza kutumika kuwahifadhi wananchi wakati wanapolazimika kuhama makazi yao kutokana na majanga. wameeleza kuwa maandalizi ya mapema, utoaji wa elimu na ushirikiano kati ya Serikali na wananchi ni muhimu katika kupunguza madhara ya majanga yanapotokea.
Na Stephen Noel.
Wananchi wa Kitongoji cha Kwa Mshango, Kijiji cha Ilolo wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma, wameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kuchukua tahadhari dhidi ya majanga, pamoja na kuweka mpango maalumu wa kuwasaidia wananchi pale majanga yanapotokea.
Wananchi hao wameyasema hayo katika mahojiano maalumu na Dodoma FM yaliyofanyika katika kijiji hicho, wakieleza kuwa elimu na maandalizi ya mapema vinaweza kusaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa majanga.
Akizungumza katika mahojiano hayo, mmoja wa wananchi hao, Elisha Maulidi, amewataka wananchi kuzingatia taarifa na tahadhari zinazotolewa na wataalamu ili waweze kuchukua hatua mapema.
“Mimi naamini kauli za wataalamu, labda Mungu aamue vinginevyo, lakini tuache kupuuza taarifa za wataalamu ili tuweze kuchukua tahadhari mapema,” amesema Elisha.
Kwa upande wake, Alex. Majaliwa amesema changamoto kubwa inayowakabili wananchi katika kuchukua tahadhari ni kukosekana kwa maeneo mbadala ya kuhamia pale maeneo yao yanapokumbwa na majanga.