Wananchi Tumbili waomba shule shikizi
20 October 2026, 16:58

Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa ziara za Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini katika kata na mitaa mbalimbali ya jimbo hilo, kwa lengo la kusikiliza maoni ya wananchi, kubaini changamoto zinazowakabili na kushirikiana na viongozi pamoja na wataalamu kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.
Na Kitana Hamis.
Wananchi wa Kijiji cha Tumbili, kilichopo Mtaa wa Chechem, Kata ya Kingale, wameiomba Serikali kujenga shule shikizi katika eneo lao ili kupunguza umbali unaotembea na watoto kufuata masomo katika Shule ya Msingi Kin’gang’a.
Ombi hilo limetolewa wakati wa ziara ya Mbunge wa Jimbo la Kondoa Mjini, Mhe. Mariam Ditopile, alipo watembelea wananchi hao kwa lengo la kusikiliza na kufuatilia changamoto zinazowakabili.
Akijibu ombi hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kondoa, Ndg. Said Majaliwa, amesema Halmashauri itatuma timu ya wataalamu kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini uwezekano wa kujenga shule hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge Ditopile ameahidi kuchangia ujenzi wa boma la shule hiyo endapo upembuzi yakinifu utathibitisha kuwa kuna uhitaji wa shule shikizi katika eneo hilo.

Katika mkutano huo, wananchi pia waliuliza kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani na namna unavyowanufaisha wakulima. Wakitoa ufafanuzi, viongozi wameeleza kuwa mfumo huo unalenga kuhakikisha wakulima wananufaika na mazao yao kupitia utaratibu wa bei elekezi.
Aidha, wakulima wanaweza kuuza mazao yao kwa wakusanyaji (aggregators), ambao huyapeleka ghalani. Utaratibu huo husaidia kupunguza ulazima wa wakulima kusafiri umbali mrefu kufuata maghala, huku wakipata malipo kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.
Akizungumzia suala la Hospitali ya Mji Kondoa kutoa rufaa za wagonjwa kwenda Dodoma, Mkurugenzi Majaliwa amewataka wananchi kuzitafsiri rufaa hizo kama sehemu ya utaratibu wa matibabu badala ya kuziona kuwa ni adhabu.
Ameeleza kuwa rufaa hutolewa pale wataalamu wa afya wanapobaini kuwa mgonjwa anahitaji huduma au uangalizi wa kitaalamu zaidi ambao hauwezi kupatikana katika kituo husika.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuajiri watumishi wa afya, huku hospitali hiyo ikiendelea kupata wataalamu wapya kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma.