Dodoma FM

Vijana wametakiwa kutumia teknolojia kuendeleza kilimo

7 October 2026, 16:42

Picha ni vijana wakiwa katika kongamano la kilimo ikolojia Tanzania 2026. Picha na Anwary Shabani.

Kongamano hilo limewakutanisha vijana, wakulima na wadau wa kilimo ikolojia kwa ajili ya kubadilishana maarifa, teknolojia na uzoefu, huku likisisitiza matumizi ya ubunifu na teknolojia katika kujenga kilimo chenye tija, ajira na fursa za biashara.

Na Anwary Shabani.

Vijana nchini wametakiwa kutumia ipasavyo teknolojia, ubunifu na maarifa katika sekta ya kilimo ili kujenga fursa za ajira, biashara na kuongeza thamani ya mazao, huku wakitumia fursa zinazotokana na mabadiliko ya teknolojia katika kuimarisha kilimo endelevu.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Kilimo, Gungu Mibavu, wakati akizungumza katika Kongamano la Vijana la Kilimo Ikolojia Tanzania 2026.

Mibavu amesema kuwa kijana mwenye maarifa anahitaji mazingira ya kutumia maarifa hayo, huku mwenye bidhaa akihitaji soko na mwenye teknolojia akihitaji nafasi ya kutengeneza na kujaribu suluhisho linaloweza kujibu changamoto zilizopo katika jamii.

Aidha, amesema teknolojia za kidijitali, taarifa za masoko na mifumo mbalimbali ya usimamizi vinaendelea kubadilisha namna watu wanavyofanya biashara na kutafuta fursa, hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha teknolojia hizo zinawafikia vijana na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika sekta ya kilimo.

Kwa upande wao, baadhi ya wakulima walioshiriki katika kongamano hilo na wanaojihusisha na kilimo ikolojia, wamesema wamejikita katika uzalishaji na uuzaji wa mbegu za asili ambazo zimekuwa zikipotea kutokana na mabadiliko ya mifumo ya kilimo.

Wamesema kupitia ushirikiano na baadhi ya taasisi za kifedha, wanaendelea na juhudi za kuhifadhi, kuzalisha na kurejesha mbegu hizo ili ziendelee kuwa sehemu ya kilimo na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakulima.

Simulizi na Anwary Shabani.