Dodoma FM

Jamii na familia zatakiwa kuacha kuwaficha watoto wenye ulemavu

13 November 2026, 15:51

Picha ni Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), wakiwa katika picha ya pamoja. Picha na Anwary Shabani.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha mifumo ya kisheria ya kulinda haki na usawa kwa watu wenye ulemavu katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku jamii ikikumbushwa kuwa ulemavu si sababu ya kumnyima mtu haki, heshima wala fursa za kushiriki kikamilifu katika maendeleo.

Na Anwary Shabani.

Wito umetolewa kwa familia nchini kuacha tabia ya kuwaficha, kuwatenga na kuwanyima fursa za elimu na haki nyingine za msingi watu wenye ulemavu, katika jamii.

Wito huo umetolewa na Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), wakieleza kuwa tayari zipo sera na sheria zinazolenga kulinda haki za watu wenye ulemavu, hivyo hakuna sababu ya familia kuendelea kuwanyanyapaa.

Akizungumza jijini Dodoma, Mbunge wa EALA anayewakilisha Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala Mtambuka, Dkt. Abdullah Makame, amesema wamepokea taarifa za baadhi ya familia kuwaficha watoto wenye ulemavu ndani ya nyumba na kuwanyima fursa ya kwenda shule pamoja na kupata haki zao za msingi.

Dkt. Makame ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa kupokea maoni ya wadau kuhusu Muswada wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 2024 (EAC Persons with Disabilities Bill, 2024), akisisitiza kuwa muswada huo ni muhimu katika kuimarisha ulinzi wa haki za watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Mbunge wa EALA, Ansar Abubakary Kachwamba, amesema ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ni hatua muhimu katika kuhakikisha muswada huo unakamilika kabla ya kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya hatua zinazofuata.

Simulizi na Anwary Shabani.